MAADHIMISHO YA SIKU YA WAZEE DUNIANI – OKTOBA 1, 2025

SIKU YA WAZEE SIKU YA WAZEE DUNIANI 2025

Posted by admin on 2025-10-06 12:33:42 |

Share: Facebook | Twitter | Whatsapp | Linkedin Visits: 40


MAADHIMISHO YA SIKU YA WAZEE DUNIANI – OKTOBA 1, 2025

Kaulimbiu ya mafunzo siku ya maadhimisho: “Mchango wa Wazee katika Kuimarisha Maadili, Ustawi na Haki za Jamii”

Ujumbe Mkuu

Wazee ni nguzo ya maadili, hazina ya hekima, na washiriki hai wa maendeleo. Ustawi wao ni ustawi wa familia, jamii na taifa. Wanastahili heshima, haki, na ushiriki kamili katika maisha ya kijamii na kitaifa.

Mambo Muhimu Tuliyojifunza

1.      Wazee kama nguzo ya maadili

i.       Kurithisha maadili mema kwa vizazi vipya kupitia simulizi, ushauri na mfano wa maisha.

ii.      Kudumisha mshikamano wa kifamilia na kijamii.

iii.     Kuongoza jamii katika maadili ya kiroho na kijamii.

2.      Ustawi wa wazee ni ustawi wa jamii

i.       Upatikanaji wa huduma bora za afya na lishe.

ii.      Ushirikiano wa kijamii ili kuepuka upweke.

iii.     Kujenga urithi wa amani, mshikamano na maridhiano kati ya vizazi.

3.      Haki za msingi za wazee

i.       Heshima na utu, bila kudharauliwa au kunyanyaswa.

ii.      Haki ya huduma za afya, hifadhi ya jamii, na kushiriki katika maamuzi.

iii.     Kulindwa dhidi ya ukatili na kudhulumiwa mali au urithi wao.

Kauli Mbiu ya Tanzania 2025

“Kuhakikisha wazee wanashiriki katika uchaguzi kwa ustawi wao”

i.       Kura ni sauti ya mzee.

ii.      Ustawi wa mzee unategemea viongozi bora.

iii.     Mzee ni mshiriki, si mtazamaji.

iv.     Ushiriki hujenga heshima na utu wa mzee.

v.      Ustawi wa pamoja ni ustawi wa familia, jamii na taifa.

Mchango wa Wazee katika Jamii

i.       Walinzi wa mila na desturi njema.

ii.      Walezi wa familia na jamii.

iii.     Viongozi wa maadili na tabia njema.

iv.     Waamuzi na wapatanishi wa migogoro.

v.      Mabalozi wa mabadiliko katika kupinga ukatili wa kijinsia.


 

MATOKEO YA MAADHIMISHO YA 2025

1.     Mahudhurio

i.       Kata ya Kwala tulifaya maadhimisho siku ya Jumatano Oktoba 1, 2025

ii.      Wazee 314 kuanzia miaka 55 walihudhuria na kushiriki mafunzo kama sehemu ya maadhimisho

iii.     Kata ya Miono tulifanya maadhimisho siku ya Alhamisi Oktoba 2, 2025

iv.     Wazee 109 kuanzia miaka 60 walihudhuria na kushiriki mafunzo kama sehemu ya maadhimisho

2.     Ombi la Wazee kwa Taifa Kupitia Equip for Change

i.       Wazee wanaomba kupewa Bima ya Afya ili kusaidia upatikanaji wa huduma za afya kwa unafuu kwao.

ii.      Wazee wanaojishughulisha na kilimo waliomba kusaidiwa mashine inayoweza kusaidia na kurahisha kazi ya kilimo kuanzia kulima, kupanda, kupalilia na kuvuna.

iii.     Wazee ambao bado wana nguvu na wanajishughulisha kijasiriamali waliomba kuingizwa kwenye mpango wa kuewa mikopo kama na halmashauri zao kama ilivyo kwa kundi la vijana na wanawake.

iv.     Wazee waliomba kupewa majiko ya Gesi asilia ili kujipatia nishati mbadala kuepuka matumizi ya kuni na mkaa ili kulinda afya zao dhidi ya moshi.

v.      Wazee waliomba angalau kila baada ya mizei mitatu wawe wanakutanishwa na kupewa mafunzo mbalimbali kama njia ya kupunguza msongo wa mawazo na kuchangamsha akili zao na mbinu ya kulinda afya ya miili yao na afya ya akili.

vi.     Wazee waliomba Serikali ijitahidi kukabili janga la ukosevu wa ajira kwa vijana ili vijana waliosoma waweze kuajiriwa na kukidhi mahitaji ya maisha yao na maisha ya wazee wao waliowasomesha

vii.    Wazee waliomba Kamari za aina zote zipigwe marufuku maana zimeua moyo wa vijana kujiajiri na kushiriki shughuli za kilimo, uvuvi na ufugaji, mambo ambayo yana tija katika kukuza uchumi ya familia na taifa pia.

viii.   Wazee walijipa jukumu la kuacha na kukemea tabia zote zinazochochea vitenda vya ukatili wa kijinsia hasa ndoa na mimba za utotoni.

ix.     Wazee waliomba Serikali iwe makini sana inapoajiri walimu kwa sababu walimu wengi sasa wameanza kuonesha tabia zinazochangia kuongeza sana kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa kwa watoto wa kike mashuleni.

x.      Wazee waliomba kila inapowezekana wawe wanapatiwa posho ya kujikimu

🌿 Hitimisho:
Wazee ni daraja kati ya vizazi. Kuwaheshimu na kuwatambua si tu kuendeleza urithi wa hekima, bali pia ni msingi wa kujenga jamii yenye mshikamano, heshima na ustawi wa pamoja.

Leave a Comment: